Thursday, December 16, 2010

NI UDINI AU OMBWE LA UTANZANIA?

 Na Jason Ishengoma,Phd
Kumekuwa na vilio na kelele kutoka kwa baadhi ya wana wa nchi hii pamoja na baadhi ya viongozi au watawala wetu kuhusu udini kama wazo au hali inayotaka kuligawa taifa la Tanzania. Nimejaribu kuona ukweli wa matamko hayo lakini hadi sasa sijaweza kufanikiwa. Mimi ni Mkristo na ninaishi na Waislamu wengi tu ambao ni marafiki wangu wa karibu na ambao tunajadili pamoja mambo mengi kuhusu mstakabali wa  nchi yetu. Kuna mengi tunakubaliana na mengi tunasigana. Hilo ni kawaida kwa watu wanaotumia ubongo na akili kujadili jambo lolote. Hajuwahi kuona kwamba matatizo ya nchi yetu yanatokana na udini. Wengine wataona matatizo yetu yanatokana na matabaka kijamii makubwa unaotokana na kuachana kimapato; wengine watasema matatizo yetu yanatokana na elimu duni ya wana wa nchi hii; nk. Mara nyingi mimi ninaona kwamba matatizo yetu makubwa yanatokana na ukosefu wa UTANZANIA kama dhana na imani inayotuunganisha wote wakazi wa nchi hii. Nchi kama nchi inafanywa na nini? Ndilo swali ninalotaka kujadili katika makala hii.
Nchi yeyote kama ilivyo Tanzania ni mkusanyiko wa jamii nyingi zenye mapokeo na simulizi (his/herstory) tofauti. Kwa Tanzania mkusanyiko huu uliratibishwa na wakoloni, kuanzia na Mjerumani miak ya1884 hadi 1920; na kumalizia na Mwingreza 1920 hadi 1961. Uratibu tulio nao sasa hivi wa inoyoitwa Tanzania, ni matunda ya makubaliano kati ya nchi mbili huru yaani Tanganyika na Zanzibar.
Kabla ya uratibu wa wageni au wakoloni, ardhi tunayokalia sasa ilikuwa na vinchi vingi vyenye dhana tofauti. Mojawapo ya dhana iliyowaweka watu wa vinchi hivi pamoja ni ile ya kuamini kwamba wana nasaba moja, wametoka kwa babu mmoja. Waliunganishwa na mapokeo hayo kutoka kwa mababu zao na taratibu wakajenga desturi, wakakuza njia za mawasiliano yaani lugha, wakawa na mila na dini zao. Wakawa watu wanaojitambua kwa mila, desturi, dini, lugha au kwa neno moja na utamaduni wao. Wakajitambua na kujitofautisha na wengine majirani zao kwa utamaduni wao, wakiwa nchi huru yenye mamlaka kamili ambayo hakuna mamlaka nyingine juu yake iliyokuwa na uwezo wa kuyahoji.
Ulipoingia ukoloni kitu cha kwanza kufanya ilikuwa kuhoji uhalali wa mababu wetu kuwa nchi. Wakaondoa dhana ya kwamba wanaamini kutokana na nasaba moja, wakaifanya dhana hiyo iwe uhalisia. Wakatuita makabila badala ya nchi na sisi hadi leo tunaendelea kukubali kwamba babu zetu waliishi kama kabila kwa maana ya uhalisia wa neno hilo badala ya kuiona kama dhana. Tumesahau kwamba wale waliokuwa wanaishi juu ya ardhi tunayoita Tanzania sasa hivi, walitoka sehemu mbalimbali, wakavyamia maeneo tofauti tofauti, wakawakuta wenyeji, au wakakubaliana kukaa pamoja au wakapigana nao na kuwashinda na kuwalazimisha washindwa kuchukua utamaduni na mila za washindi. Katika yote hayo, kumekuwako mchanganyiko wa mila; moja ikaimeza nyingine na kuwaweka waliomezwa kwenye imani ya kwamba wote wametokana na mababu walewale.
 Walipofika Wakoloni wa Kijerumani, jambo la kwanza walilofanya ni kuwaondolea wana wa nchi hii uhalali wao wa kujiongoza. Wakavunja tawala za kijadi, hasa baada ya kuona viongozi wa kijadi wakipingana nao, wakaleta utawala mpya na kuwaajiri wanyampara kwa mtindo wa maakida ili wawasaidie kuwatawala wenyeji. Nchi nyingi zilizokuwa juu ya ardhi hii, zikavunjwavunjwa na kuunda himaya mpya ya Ujerumani ya Afrika Mashariki. Udharimu huu uliwaudhi sana mababu zetu wakaamua kupigana. Mojawapo ya mapigano hayo ni vita vya Mkwawa, vya Majimaji, na vingine katika maeneo mbalimbali ya ardhi hii. Utawala wa Kijerumani uliondoa utawala wa kijadi, ukaweka utawala wa kigeni wa moja kwa moja. Baada ya vita ya kwanza ya dunia, utawala wa kijerumani ulichukuliwa na Waingereza.
Hadi mwaka 1926 Waingereza walitumia mtindo walioukuta. Mwaka huo Sir Donald Cameron alipofika Tanganyika akitokea Nijeria, alibadilisha mtindo huo na kurudisha ule wa kijadi unaokubaliwa na wenyeji. Wakawa na mtindo wa kutawala kwa kupitia watawala wa jadi. Pale ambapo utawala wa jadi haukuwa umekomaa na kuzoeleka, wakalazimisha uwepo. Wakaunda mabaraza ya Watemi wa sehemu moja na kuwapa maelekezo namna ya kukusanya kodi na kutekeleza maelekezo ya wakoloni. Hadi mwaka 1929, Tanganyika ilikuwa tayari ina mtindo wa tawala kijadi. Sehemu ambazo hazikuwa na jadi inayounganisha makabila, hasa sehemu za pwani kama vile Lindi na Mtwara, ambako watu wake walitokana na vikundi vingi vidogo vidogo vya makabila tofauti toka sehemu mbalimbali za bara, walitafuta kile kilichowaunganisha wote na kuweka utaratibu huo kama utawala wa sehemu hizo. Hizo sehemu, ndio waliwekewa mahakama za kadhi kama mahakama za kijadi za wakazi wa sehemu hizo. Kwa kurejesha utawala unaozingatia jadi na tawala za wananchi Mwiingereza hakupata upinzani mkubwa Tanganyika. Tunachokiona hapa ni kwamba uratibishaji wa nchi ya Tanzania umepitia hatua na mifumo tofauti ya ukoloni.
Baada ya uhuru, chama cha TANU, kilikuwa na mkakati wa kujenga nchi. Wimbo wa “TANU yajenga nchi” inabidi ueleweke katika mtazamo huo. Tanganyika iliyokuwa imejengwa na wakoloni haikuwa na kitu kinachoiunganisha zaidi ya ardhi na adui zao wageni wanaowatawala na kuwabagua. Viongozi wa TANU waliona umuhimu wa kujenga nchi. Wakajenga chama chenye IMANI 10. Tuliimba na kuaminishwa kwamba; “binadamu wote sawa”; “kila mmoja anastahili heshima” nk. Tuliokuwepo wakati huo tukafundishwa imani hizo ambazo ndizo zilimfanya mtu awe mwana TANU na kwa njia hiyo awe mpigania uhuru, utu na mstakabali wa Taifa linalojengwa. Ikumbukwe kwamba TANU iliridhi mtindo wa utawala wa kikoloni ambapo watemi ndio walikuwa watawala. Utawala wa kitemi haukuwa wa kuchaguliwa bali wa kuridhi.
Mwaka 1963, naukumbuka sana maan babu yangu alipoteza utemi wake akawa mtu wa kawaida. (hoi poloi) TANU ilivunja utawala wa kitemi na kuweka utawala wa kuchaguliwa. Tukawa na mabaraza ya kuongoza watu yaliyochaguliwa na watu au raia wenyewe. Hapo ndipo mahakama za kijadi, pamoja na zile za kadhi ambazo zilipatikana sehemu za pwani tu; zilivujwa na kuwekwa mahakama za mwanzo. Nia ya kuvunja tawala na mahakama za kijadi ilikuwa ni kujenga UTANGANYIKA au UTANZANIA. Azimio la Arusha lililofuatia miaka mitatu hivi baadae lilikazia misingi na imani hiyo ya Utanzania. Je kwa sasa bado imani hiyo inafundishwa kwa watu wetu? Je kama tumeigaya badala yake tumeweka nini? Siyo Ombwe?

Ninaamini sana kwamba ili kuikomboa Tanzania tunahitaji vitu viwili vikubwa: Utanzania na Wauumini wake na Wapiganiaji wa imani hiyo. Ili kufanikisha adhma hiyo tunatakiwa:
  1. Kujenga imani ya Utanzania.
  2. Kujenga wauumini wa kutetea imani yao.
Imani ninayosema ni kujenga tunu kitaifa. Tunu (values) hizo ambazo ni TAKATIFU kwa kila muumini wa Utanzania zitajengwa kwa mijadala ya kifikra kuhusu yale ambayo kwetu ni ya msingi na mtu yeyote yule anayeyagusa na “apigwe mawe”. Bahati nzuri Tanzania tuliwahi kuwa na imani Fulani, tunu kitaifa: Usawa katika Ujamaa na Kujitegemea. Tunu hizi hazina imani za kidini, ni tunu za kilei. (secular values)

Hapa kwetu ni kama vile siasa zetu ziko kinyume na zile za magharibi. Kwetu ujamaa [hapa natofautisha Ujamaa na Ujamii (socialism)] ndiyo mapokeo (tradition); ndiyo conservative. Ubepari, kama tunao, ndiyo liberals. Watu hawako tayari kupoteza yale ambayo waliyapata na kuahidiwa huko nyuma: huduma muhimu za jamii.
Tatizo lililokuwepo ni ufinyu wa kutumia akili katika kufikiri na kutafakari. Wananchi hawana mbinu za kuwabana watawala wao. Tunabaki kulalamika tangia watawala hadi watawaliwa. Inatubidi tujenge tunu kitaifa: mambo ambayo ndiyo msingi wa kuwa Mtanzania. Mambo hayo ya msingi yanapaswa kuhusisha Usawa kwa raia wote, na siyo usawa wa kimakundi kimaslahi. Tunapoanza kuhesabu ni Waislamu na Wakristo wangapi katika nafasi ya utawala, tunapoanza kuangalia ni watu wa kabila lipi katika nafasi fulani, hizo ni dalili za kutokuwepo utaifa: Umoja.
Utanzania ni lazima uwe na misingi ya umma, (dola kiumma) kutoka kwa wananchi (raia) kwenda kwa dola taifa; na papohapo liwe na misingi kitaifa, kutoka juu (kwenye dola taifa) kwenda chini kwa umma. Umoja wa umma unaounganishwa na historia moja, lugha moja na utamaduni mmoja unabaki ndiyo muhimili wa maamuzi yote na kiini cha demokrasia.

La pili ni Kujenga wauumini wa kutetea imani yao. Ukiishajenga imani ya Utanzania, ukaonyesha na kuweka wazi yale yasiyopaswa kuguswa na yeyote katika nchi hii (the UNTOUCHEABLES), ni budi kuwaandae vijana wa kulinda imani hiyo. Tunawaandaa siyo kwa kuwaweka kwenye kambi za kupata ukakamavu, bali kwa kuwafunda namna ya kutumia ubongo wao badala ya makamasi ili kufikiri. Tunawafunda kufikiri. Kufikiri ambako, ingawa ni kipaji cha mtu kinachomtofautisha na wanyama wengine, siyo kazi rahisi. Ni kazi inayohitaji mtu ajitambue na aone umuhimu wake. Kufikiri ni kukataa uhiki wa hiki. Ni kukataa kwamba hiki si hiki bali ni kingine. Matokeo ya kufikiri ndiyo yanatufanya tuunde maneno. Maneno ambayo bila kuwa nayo hatuwezi kuwasiliana lakini ambayo si tunda la Muumba bali ni tunda la watu wanaokaa pamoja na kujua umuhimu wa kuwasiliana siyo kwa kuonyesha kwamba hiki ni hiki bali kwa kuonyeshana kwamba hiki ni kitabu; (logos), kile kinachounganisha wewe ulioko kule na mimi niliyeko huku; kwa maana ya neno la kiyunani la legei. (hukusanya).
Tumebahatika kuwepo na shule za kata. Elimu inayotolewa katika shule hizo, na katika shule nyingine za kitanzania, elimu ya kukariri kwa ajili ya kushindan mitihani, haiwezi kutukomboa. Tunahitaji kutumia zana tulizo nazo, kuunda Tanzania mpya. Huu siyo mkakati wa serikali. Wote tunajua kwamba serikali haiwezi kuwafunda vijana waihoji. Hii ni kazi yetu wengine hasa asasi za kijamii. Kazi imeishaanza ya kuwaamsha wananchi, Haki Elimu kwa mfano wanafanya kazi kubwa na lile ninalolizungumzia. Bali bado hawawatayarishi waumini wa kupigania imani yao. Asasi zinazohamasisha Utanzania zianze, ziende kwa wananchi, kwenye mashule ya kata, kwenye vikundi vya vijana nk. Hakuna sheria inayokataza kuunda vikundi vya mwamsho katika nchi yetu. Tuunde vikundi hivyo na tuvipe nyenzo za kufikiri kitunduizi ili wao wenyewe wapate jawabu la maswali yanayohusu maisha yao. Hakuna chama cha siasa wala kikundi cha dini kinachweza kutoa majibu kwa maswali yanayohusu maisha ya mwananchi. Wananchi wenyewe, kwa kuhamasishwa na kujitambua kwamba wana nguvu na uwezo, kwamba wenyewe ndiyo wenye dola, wataamka na kudai wanachokitaka. Bila kufanya hivyo, tutaendelea na vikundi vya kiimani ambavyo havina utaifa wowote, ambavyo badala ya kutuunganisha vinatutawanya. Ndiyo maana katika kampeni za mwaka huu, kwa vile tumefirisika kifikra, mawazo ya udini yalitawala.
Kwa leo namalizia kwa kusema: Utanzania haujajengwa kwa ufasaha, haujafafanuliwa ukaeleweka. Wapambanaji hawajatayarishwa. Tunahitaji mwanga mpya. Tutoke maofisini na mezani kwetu turudi kwa watu, tukae nao, tule nao, tufikiri nao. Tutoke ughaibuni tulikopelekwa na elimu isiyoakisi mazingira yetu. Hapo ndipo ufahamu wetu, elimu yetu, maarifa yetu, na upeo wetu utakapopata kipimo sahihi.  TUAMKE.



3 comments:

  1. Asante kaka kwa changamoto.

    ReplyDelete
  2. Huoni kuna umuhimu kuchambua kwanini Waislamu na jamii zingine zinasema kwamba kuna uhaba wa elimu, afya, na huduma nyingine bora? Kwangu mimi suala sio la utaifa pekee bali ni kwamba wananchi wana ukosefu gani na ni katika haya mapungufu ndio hitilafu kama hizi zinatokea.

    ReplyDelete
  3. Nakubaliana na msemaji hapo juu Wananchi wakisema kwamba wanabaguliwa kwenye nyanja za elimu, afya, na malazi, kwanini tusichunguze kwa undani na kuweka sera na tafiti kuchambua zaidi. Mimi sioni hili suala kama ni la uzalendo tuu hili ni suala la huduma pia.

    ReplyDelete