Sunday, October 24, 2010

KWA WALIMU WOTE

Sikilizeni walimu wenzangu mwito kutoka kwa Mwalimu mwenzetu. Mwito wa kututoa katika dimbwi la usingizi. Nadhani ni Mwalimu tu anayeweza kujua na kueleza kilio cha wenzie. Tumsikilize kwa makini Mwl. E. Kezilahabi. Haya siyo maneno wala mawazo yangu. Ni mawazo ya Mkereketwa anayefikiri juu ya hatima ya nchi isiyojali wakunga wake: Walimu.


Sikilizeni wimbo huu:
Nilipokuwa mtoto niliitwa Chacha
Kwa matamshi yangu ya sasa
Nilipokuwa kijana niliitwa Chaupele
Nilipokuwa mtu mzima niliitwa Manywele
Nilipokuwa Mwalimu nikaitwa Bure.

Huu utakuwa wimbo wako
Utakapostaafu urudipo nyumbani
Umelewa kangara na nyayo zako
Zikishindwa kulenga njia nyembamba vijijini.
Utakuwa kichekesho cha watoto
Watakaokuita, Ticha! Popote upitapo.

Kumbuka Mwalimu utakapostaafu.
Mijusi watataga mayai ndani ya viatu
Vyako vilivyokwisha visigino
Na ndani ya sidiria chakavu
Zilizoshikizwa kamba kwa pini.
Mende watazaliana ndani ya chupa tupu
Za marashi na za bia.

Na manyigu yatajenga ndani ya kofia
Zilizosahaulika kutani.
Utakapokufa nge watazaliana
Chini ya jiwe juu ya kaburi lako,
Na mlevi fulani (isome fisadi) akipita atapenga
Na kupangusa vidole kwenye jiwe pweke.
Mwanzo na mwisho wako ndio huo.

Lakini wakati ungali hai
Unaweza kubadilisha mkondo wa maji.
Lakini kwanza tuzungumze. Wewe na mimi.
Acha mioyo yetu izungumze.
Baada ya kunyanyaswa
Na kisha nusu mshahara.

Utafundisha tena nyimbo kuwasifu viongozi?
Utafundisha tena ngonjera?
Utapeleka tena wanafunzi asubuhi
Wakijipanga barabarani kusubiri
Mgeni afikaye saa kumi, na apitapo
Apunga tu mkono kuwatia kichaa cha shangwe
Na huku nyuma mwasambaa na njaa?

Tazama hilo rundo la madaftari mezani
Utamaliza kwa mshahara mkia wa mbuzi?
Tuzumgumze. Ninyi na mimi.
Acha mioyo yetu izungumze.
Mkiwa waoga na kujikunja kama jongoo
Mtawekwa kwenye vijiti na kutupwa
Nje ya ua, na ndani mtawaacha
Wacheza ngoma wakitunga nyimbo mpya.

Sikilizeni walimu.
Anzeni kufundisha hesabu mpya:
Mjinga mmoja kujumlisha na wezi (mafisadi) ishirini
Ni sawa na sifuri.
Fundisheni historia mpya:
Hapo zamani za sasa
Hapakuwa na serikali.

Sikilizeni kwa makini.
Umoja hatuna:
Twasambaratika kama nyumbu.
Tulichonacho ni woga,
Na kinachotuangusha ni unafiki.
Lakini tusikate tamaa kama mbuni.
Tukiupata umoja bado tunayo silaha.
KURA.

(Kezilahabi, Dhifa, Vide-Muwa publishers, Nairobi. 2008)

Walimu wenzangu, tunalipeleka wapi taifa kwa woga wetu? Kweli tunaliunda taifa la kesho la kuigwa? Kwa nini tunafanya mauaji kwa taifa tukijua kweli kwamba tunayofundisha hayawezi kuwapeleka watoto wetu popote na hii inasababishwa na mafao duni yanayotufanya tukimbilie mitaani kutafuta riziki ya kutufikisha mwisho wa mwezi? Tunayo silaha, katuasi Mwalimu mwenzetu. KURA

Jason Ishengoma,Phd

No comments:

Post a Comment