. “Uhuru hupatikana kwa kuutoa uhai wako.(kujitoa mhanga) Mtu ambaye hajathubutu kujitoa mhanga, yaani kuutoa uhai wake, anaweza kweli kujidai kwamba anatambuliwa kama mtu, lakini hakufikia ukweli wa utambuzi huo kama nafsi huru inayojifahamu.”
(Phenenomelogy of Spirit. # 187)
Maneno hayo nimeyanukuu kutoka katika kitabu cha mwanafalsafa wa kijerumani, Hegel kutoka katika kitabu cha “Mwonekano wa Roho”. Hegel aliandika kitabu hicho wakati mabomu ya Napoleon Bonapatre yanalindima katika mji wake wa Stuttgart 1807.
Vita vya Napoleon vilikuja baada ya Mapinduzi ya Ufaransa ambayo yaliwatimua watawala wa nchi hiyo iliyoongozwa na mfalme Louis wa 16. Pamoja na kwamba mfalme huyo alikuwa na maaskari na vifaa vya kumlinda, hakuweza kushindana na nguvu za umma uliochoka kwa udhalimu na ukandamizaji pamoja na maisha magumu yaliyotokana na maisha ya anasa ya watawala wa wakati huo.
Tumo katika kipindi cha kuelekea uchaguzi. Ni kipindi ambacho tunaambiwa ni muhimu katika utekelezaji wa kile ambacho wale waliotufinyanga wanakiita Demokrasia. Kwao hao Wafinyanzi wetu demokrasia ina maana ya utawala unaotokana na wengi badala ya wachache wanaojiona kama vile ni wateule wa Mungu. Tunaaminishwa kwamba demokrasia ni ya wote na katika utekelezaji wake baadhi wanaweza kuwakilisha wengi.
Hayo yote sina ugomvi nayo maana tumo katika mkondo wa kileo au kisasa. Tatizo langu ni pale ninapotaka kuswali namna tunavyolielewa wazo zima la demokrasia. Katika nchi yetu kumekuwa na mfumo unaoifanya nchi iwe kama kaya, na yule anayepewa kuongoza nchi, na siyo kutawala, anajiona kama mkuu wa kaya. Kuelewa, kutumia na kuendekeza dhana ya kiongozi wa nchi kama baba mwenye nyumba ni kurudisha nyuma fikra zetu na kutotaka kuelewa nchi au dola ina maana gani katika fikra zetu Waafrika na hata katika fikra za wafinyanzi wetu. Baada ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhutubia wazee wa Dar-es-Salaam kwa ukali kuhusu mgomo wa wafanyakazi uliotaka kuitishwa, baadhi ya Watanzania walitafsiri hotuba hiyo kama ya baba mwenye nyumba ambaye amekasirishwa na watoto wake. Kwa fikra zangu, hata raisi mwenyewe alipokuwa akihutubia alifikiri anawahutubia walio chini ya himaya yake. Hakuhutubia kama vile wale ni wabia wenzake waliopewa majukumu tofauti na mwajiri namba moja yaani UMMA.
Fikra hizi za kuona nchi kama mwendelezo wa kaya, na napenda kutumia neno kaya na siyo familia, zimo katika vichwa vya watu kwa muda mrefu sana. Plato katika maandishi yake ya “Republic”, anaiona nchi kama mwendelezo wa kaya. Ndiyo maana anaona mpangilio wa nchi au dola lazima ufuate ule wa kaya. Baba ni kichwa na mfikiriaji; mama ni kifua chenye upendo anayewalea watoto; watumwa, ambao wakati huo walikuwa sehemu muhimu ya kaya, ni miguu na mikono ya kufanya kazi ili kila mmoja apate riziki yake. Kwa mawazo ya Plato nchi inapaswa kuwa hivyo: ni kaya kubwa zaidi. Kila mmoja kwa nafasi yake kadri ya uwezo alio nao. Si Plato tu, Mwalimu Nyerere katika falsafa yake ya Ujamaa hayuko mbali na Plato. Anatumia dhana ya kiafrika ya kaya, ambayo anaisimika katika neno la Kiswahili jamaa linalotoka katika lugha ya kiarabu, na kulitumia kama dhana ya falsafa ya siasa ya kiafrika.
Fikra hizo ziliendelea kutawala kwa muda mrefu hadi yalipojitokeza Mapinduzi ya fikra na siasa ya kileo ambapo dhana ya Kujiendesha (uhuru) inatawala. Katika dunia ya leo ambayo ilijionesha dhahiri katika ulimwengu wa kimagharibi kwa Mapinduzi ya Ufaransa, fikra ya kujiendesha, na siyo kujitawala, ndiyo mhimili na maelezo ya maisha ya watu.
Kwa nini fikra ya kaya haiwezi kuhimili vishindo vya fikra za kileo? Kaya ni mkusanyiko wa watu ambao unatokana na ulazima wa uhalisia au maumbile kinyama. Watu kama watu, [na siyo kwa kuwaita Bin Adam kama vile Binti Adam hawana lao katika kusanyiko hilo], huanza mkusanyiko wa kikaya kwa vile maumbile yanawavuta mwanamume na mwanamuke, wote kama wana au watoto, waunganike. Muungano huo siyo wa hiari. Ni muungano wa kimaumbile, wa lazima. Katika muungano wao huo, huzaa watoto ambao nao aidha ni wake au ni waume. Muungano wa kikaya, ni muungano wa lazima siyo muungano wa kujiendesha (huru). Fikra ya kujiendesha haiwezi kuwemo katika fikra ya kaya. Katika kaya hakuna utashi; kuna ulazima. Hakuna aliyechagua kuzaliwa katika kaya fulani, hakuna anayechagua baba au mama au kaka au dada. Unajikuta katika kaya hiyo na hauna utashi wala uchaguzi.
Katika dunia inayoendeshwa na dhana ya kujiendesha, dhana ya kaya inapotosha ukweli na kufanya fikra zetu zigande. Na katika mgando-fikra huo wa kutotaka kudadisi, kuchambua na kupekuapekua masimulizi (historia), watawala wetu wanapata mwanya wa kujifanya miungu na kututawala. Tunachohitaji katika nchi inayojiendesha, ambayo kwa maneno ya kila siku mmaiita huru, ni viongozi, wanaotuongoza kuelekea kule tunakotaka kuelekea: wanaosimama na sisi wakiwa mbele katika kujiendesha na siyo kuendeshwa. Uongozi huo unawezekana pale ambapo watu wanaojiendesha wanachagua viongozi wao kwa uhuru. Uchaguzi wa namna hiyo unatokana na UTASHI.
Lakini maisha hayaendeshwi kwa utashi tu. Utashi hauwezi kulima “ulime”, utashi hauwezi kujenga nyumba. Tunahitaji akili pia. Akili, hudadisi, hushakia, hugundua, huhesabu. Akili hupanga. Akili haichagui. Taswira ya akili ni kuona jinsi kitu kilivyo. Akili haiwezi kuchagua kati ya hiki au kile itaona kama ni sawa au si sawa na wala si kama ni kibaya au kizuri. Haiwezi kutaka kufanya jinsi inavyotaka. Akili huogozwa na uhalisia wa kitu kwa jinsi inavyokiangalia na kukiona. Akili inatumika katika kupanga, kutenda jambo au kufanya kitu. Wale wanaotumia akili katika kutenda au kufanya jambo tunawaita Wata-alamu, yaani watu wa taaluma. Utaalam unatokana na elimu inayoleta ujuzi au ufundi, yaani namna ya kufunda vitu; yaani, kuvifanya vitu viwe na umbo au fundo. Katika jamii inayojiendesha ni lazima kwanza mtu ajue anaweza kufanya nini ili kuendesha maisha yake. Anaweza kulisha vipi kaya yake kwa kuzalisha chakula cha kutosha kipindi chote cha mwaka. Anahitaji kutumia akili. Kwa kutumia akili hiyo hiyo, mtu anaona mipaka yake. Anaona kwamba hawezi kwenda mbali kwa kukaa na kaya yake peke yake. Anahitaji kaya nyingine, anahitaji ufundi na ujuzi wa mwingine ili aweze kupata kile anachokitamani na kukipenda. Hapo anatumia utashi wake kuchagua kushirikiana na wenzake ambao siyo wa kaya yake bali wenye kaya zao ili wote kwa pamoja wafikie kile ambacho kila mmoja anakitamani lakini hawezi kukipata akiwa peke yake. Akili inamfanya mtu aone uhalisia wa vitu na utashi unamfanya achague njia ya kufuata ili kufikia lengo lake. Lengo ni kile unachokitamani, kile unachotarajia. Hicho ndicho unachokichagua.
Katika utashi ndimo demokrasia imejikita, ni kuchagua. Uchaguzi unahusu kuchangua wale watakaotuongoza na wala siyo wale watakaotutawala. Kuongoza ni kuonesha njia. Huwezi kuonesha njia kama hujui unapokwenda yaani unapoelekea. Kuishi kwa kujiendesha yaani kwa uhuru ni kujua unakotaka kwenda na kutafuta njia ya kukufikisha kule Ili kuwa na viongozi tunahitaji kujua lengo la watu husika. Kujua njia kunahitaji kutumia akili, siyo utashi. Viongozi pamoja na wale wanoongozwa wanahitaji WAONESHAJI, wanaojua njia ilivyo. Hawa ni Watawala (administrators) na wala siyo viongozi (Leaders). Watawala wana uwezo wa kudhibiti, kufanya vitu viende kwa utaratibu fulani. Wanajua njia, ni wataalam. Lakini je, watu kama watu tunaweza kuwaachia wataalam, watu wanaotumia akili yao tu, kutuonesha kule tunakotaka kwenda bila kuwadhibiti?
Katika ushirikiano wa kileo hilo ndilo lililozaa mgawano wa madaraka katika jamii kati ya Uongozi ambao unapewa Serikali na Utawala ambao unafanya kazi chini ya serikali. Serikali ya watu wanaojiendesha wenyewe, ni serikali inayotokana na watu. Inachaguliwa. Inapochaguliwa serikali hiyo inakabidhiwa watawala, yaani wataalam wa nyanja mbalimbali ili wawafanyie kazi WENYEDOLA, yaani wenyenchi, na siyo tu wananchi, kwa malengo waliyokubaliana. Viongozi wanaokabidhiwa serikali wanawakirisha matakwa au utashi wa wenyedola. Serikali haina dola, inakabidhiwa vyombo, ili ivitumie vyombo hivyo kwa niaba ya wenyedola.
Vyombo vya dola ni vyombo katika maana kamili ya vyombo. Havina utashi wala mamlaka ya kufanya vinavyotaka. Vinafuata matakwa ya wenyedola ambao ni raia wa dola hilo. Lakini katika tabia na mazoea tuliyojiumbia, vyombo vya dola vinaanza kujiona kama vile viko juu ya wenyedola. Kuwaonesha wenyedola mbinu za maguvu ya kuwatishia kama watadai haki yao ya kuchagua wale wa kukabidhiwa mikoba ya kuendesha dola, ni kwenda kinyume na uongozi wa kujiendesha. Wataalm wa kutumia dhana za kudhibiti adui wa dola (jeshi) wako chini ya wenyedola. Jeshi halina nguvu juu ya UMMA. Adui wa umma ni adui wa dola. Na jeshi linalotishia umma limeacha kuwa chombo cha dola. Utawaua raia wangapi wanapoanza kupigana wenyewe kwa wenyewe? Jeshi utakuwa wapi? Nje ya umma au sehemu ya umma?
Serikali yoyote ni mali ya umma, ni mali ya wenyedola. Lakini tumekuwa na kasumba ya kuchanganya serikali na umma. Hata vyombo vya umma, kama vile wafanyakazi, badala ya kuitwa watumishi wa umma (civil SERVANT); watu wa kutumwa na umma, tumewaserikalisha na kuwaita wafanyakazi wa serikali. Tukumbuke kwamba serikali inabadilika kila baada ya uchaguzi. Je? Wafanyakazi hao uwa wanabadilisha mwajiri kila baada ya miaka mitano? Je wafanyakazi wa serikali, wanaajiriwa na nani wakati serikali mpya inapoundwa? Serikali huondoka lakini umma hubaki. Watawala wetu, yaani watumishi wa umma, wangejifunza hilo kwamba anayedumu ni umma na wala siyo serikali, tungepiga hatua. Tungeachana na vitisho tunavyopatiwa wenyedola ambao tumenyanganwa dola au nchi yetu na tukabaki ni wana wa nchi tu: WANANCHI. Tumebakiza haki ya kuzaliwa tu ambayo kama nilivyogusia hapo juu haitupi nafasi ya kujiendesha, yaani kuwa huru. Ni ulazima tu kwamba ni wana wa nchi hii.
Tabia yetu tuliyojijengea ya kuangalia mambo bila kuyadadisi na kuyashakia, ndiyo inayotufanya tutawaliwe na watawala wanaotufanya ni watoto na wao ni baba. Hali hiyo hiyo ndiyo inatufanya watumishi wa umma tujione ni sehemu ya uongozi ambao umejifanya utawala. Mtumishi ni mtaalam, amewekwa pale na wenyedola ili atumike kwa sababu ya utaalam wake na siyo urai wake. Serikali inaongoza wenyedola kwa kupitia watawala ili watawale njia. Lakini kule tunakoelekea tunapataka sisi na wala siyo serikali wala watawala.
Serikali yoyote ni wapangaji katika nyumba inayoitwa taifa na siyo wenye nyumba.
Tuifungue akili yetu ione na iwe huru ili tujiendeshe kuelekea kule tunakakotaka.
Swali: je taifa la Tanzania linataka au linaelekea wapi? Labda kwa kuwa hatuna dira, hatuna mwelekeo, hatujui nani mlenga shabaha mzuri anayeweza kutufisha pale.
Kama mwanafikra nabaki nikiranda katika msitu wa kufikiri: je taifa letu lina Watu ambao kwa mtazamo wa Azimio la Arusha ndiyo msingi wa kwanza wa maendeleo? Je hatuna mkusanyiko wa watu ambao hawana muono wa pamoja hivyo kila mmoja anajali kaya yake na tumbo lake? TUTAFAKARI!
By Dr. Jason Ishengoma.
No comments:
Post a Comment