Sunday, October 24, 2010

TUNAMTANZANISHAJE MTANZANIA?

“Ili tuendelee tunahitaji vitu vinne: WATU, ARDHI, SIASA SAFI NA UONGOZI BORA”


Maneno haya yaliyoandikwa na waasisi wa Azimio la Arusha. Tuliyaimba na kuyakariri kama kasuku enzi za ujana wetu. Tuliaminishwa na kufahamishwa kwamba hayo manne ndiyo misingi ya maendeleo. Kwamba tuliyakubali na kuyaelewa hayo hilo ni jambo lingine, ila ukweli ni kwamba tulifundishwa na kutakiwa kuamini hayo. Mimi binafsi bado ni muumini wa misingi hiyo ya maendeleo ya taifa ambalo linataka maendeleo ya watu kama alivyotufundisha Baba wa Taifa, na siyo ya vitu.

Mengi yameandikwa na kufanyiwa utafiti juu ya misingi hiyo ya maendeleo. Tunajua mengi kuhusu utajiri tulio nao juu ya ardhi yetu na chini yake; tunajua hata utajiri ulioko majini kama ziwani na baharini. Wasomi wanajua na wanafanya utafiti juu ya siasa na uongozi unaofaa kwa ajili ya nchi yetu kwa kipindi hiki cha soko huria. Tunajua mengi na tunatafiti mengi juu ya misingi hiyo ya maendeleo. Lakini je tumeweza kujiuliza kama kuna watu ambao maendeleo hayo yanawalenga au tunachukulia kivyepesivyepesi kwamba wapo ili mradi tunayo idadi fulani ya wakazi juu ya ardhi hii? Kinachomfanya mtu awe Mtanzania ni nini? Ni kule kuzaliwa na kukulia kwenye ardhi ya nchi inayotambuliwa kwamba ni Tanzania? Je mtu huzaliwa akiwa raia wa nchi fulani au hufundwa kuwa raia wa nchi husika? Hayo ni maswali yanayonitinga ninapotafakari mstakabali wa nchi yetu.


Mimi si shabiki wa siasa za kivyama. Mara ya kwanza na ya mwisho kuhudhuria kampeni za kisiasa kabla ya mwaka huu, ilikuwa ni mwaka 1975 nilipokuwa napiga kura kwa mara ya kwanza. Kulikuwa na wagombea wawili mmoja ana alama ya jembe na mwingine ya nyumba. Sikumbuki nilimpigia kura mgombea yupi kati ya hao wawili. Wakati huo nilikuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama kwa tiketi ya Vijana wa TANU, tawi la Kaisho kule Karagwe. Hizo zilikuwa siku za ujana wangu ambapo nilipikika nikaiva kisiasa. NiliTANUishwa, nikaTANZANishwa. Nikapewa mafunzo na maono kuhusu nchi yetu. Watanzania wote, wake kwa waume, vijana kwa wazee, tulioneshwa lengo: Ujamaa na Kujitegemea. Tuliambiwa tusiwe kupe kuwanyonya wengine ili tuishi, bali tujitegemee. Tulipewa matumaini kwamba kwa pamoja tutafika kule tunakotaka kufika kwenye Ujamaa na Kujitegemea. Tulipewa shauku na hamu ya kuishi ili tufike huko. Tulijivuna kuwa Watanzania.

Wakati huo yule aliyetayarishwa kumtanzanisha mtoto wa kitanzania (Mwalimu) hakupelekwa kwenda kusoma kwenye Chuo cha Ualimu kama ilivyokuwa zamani kabla ya kuzaliwa taifa la Tanzania, bali alipelekwa kwenye Chuo cha Elimu ya Taifa. Ajifunze namna ya kumpa fundo mtoto wa kitanzania la kuwa Mtanzania anayeishi na wengine kwa kufanya kazi inayomfanya ajitegemee. Wakati huo tulitambua umuhimu wa elimu inayomkomboa mtu kwa kumfanya ajitambue yeye ni nani na pale pale awatambue wengine ambao si kama yeye bali na wao wapo katika uso wa dunia hii. Je? tumerudi kulekule kwenye chuo cha ualimu ambao hauna utaifa?

Maendeleo ni ya Watu na si ya vitu, anatuasa Mwalimu. Ni mtu wa namna gani ambaye anaweza kuhodhi maendeleo? Kwa maoni yangu, ni yule ambaye amefahamishwa, akapewa uwezo wa kuchanganua, kushakia yaani kutilia shaka kile anachokiona na kuambiwa ili apate kujua kwa kutumia ubongo wake uliochemka na siyo ule ulioganda kwa mapokeo ya kwa kuambiwa tu. Ni yule ambaye anajua anachojua na kujua ujinga wake yaani kile asichokijua. Huko ndiko kuondokana na ujinga ambao enzi za Mwalimu hakukuishia darasani bali ilikuwa ni kazi ya maisha yote. Kisomo chenye manufaa (cha watu wazima) kilitaka kuleta changamoto hiyo!

Kuhesabu vyumba vya madarasa, barabara za lami n.k, ni safi kabisa. Lakini je, wenye hizo barabara na shule wanajua kwamba ni zao au wanaaminishwa kwamba ni kazi ya serikali? Elimu ya kweli inapaswa kumwonesha, kumfahamisha raia, (na siyo mwana wa nchi,) kwamba vile vitu ni vyake: vimetokana na juhudi zake, na utashi wake wa kutaka kutoka pale alipo ili afike pahali pazuri zaidi. Je Mtanzania wa leo anajua na kuamini kwamba hivyo viashirio vya maendeleo ni vyake? Au anaamini na kuaminishwa kwamba vimeletwa? Kama vitu hivyo vinavyoashiria maendeleo vingekuwa vya watu, watu wale wasingekuwa wanaomba serikali iwajengee shule, iwajengee barabara, iwaletee maji nk. Wangepanga wenyewe, wakaamua wenyewe na kuitaka serikali (siyo kuomba) itekeleze hayo. Kwa raia ambao wamefundwa, hiyo ni haki yao ambayo wanatakiwa kuidai, na kwa serikali inayotokana na watu (raia) huo ni wajibu wao ambao wanatakiwa kuutimiza.
Yote haya yanawezekana kama tuna elimu inayomfanya mtu (Mtanzania) ajitambua. Atambue yeye ni nani? Kwamba ni raia wa nchi hii, mwenye wajibu na haki ya kuishi, kufanya kazi na kushirikiana na wenzake kwa manufaa yake binafsi na yale ya taifa lake. Huo ndiyo msingi mama wa elimu, uhuru na maendeleo: KUJITAMBUA (self-consciousness)

Inasikitisha kufuatia kampeni zetu za kisiasa. Kuna vijana wengi ambao wanahudhuria kampeni hizo. Lakini nyingine ni burudani tu. Badala ya kuwaamsha watu ili wajitambue kwamba sasa ni wakati wao kama raia wa kupanga mstakabali wa nchi yao, kwamba nchi inawategemea wao kuijenga, kuchagua nani wa kuwaongoza kuelekea kule ambapo wanaoneshwa; wanaimbiwa ngojera za kuletewa maendeleo. Tangu lini maendeleo ya watu yakaletwa kwa watu?
Najiuliza hivi kweli tunawatendea haki vijana wa nchi hii? Je tunawapa elimu inayowakomboa ili wadadisi mambo, wawe watundu wa fikra kwa kutunduiza fikra? Sina uhakika.

Bila kuwapa hayo: matumaini, maono na taswira; vijana wetu watatupiga mawe kwa haki kabisa. Tunawaboa!

Na Jason Ishengoma,Phd

No comments:

Post a Comment